MKUU WA CHUO KIKUU MZUMBE ATOA HAMASA KUHARAKISHWA UJENZI ENEO LA IWAMBI - MBEYA

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Barnabas Samatta ameendelea na ziara yake ya kukagua maendeleo ya chuo hicho kwa kutembelea Kampasi ya Mbeya na kufurahishwa na maendeleo makubwa upande wa Taaluma na miundombinu.

 Akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Prof. Matthew Luhanga, na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka; Mkuu huyo alipata fursa ya kupitia mpango wa matumizi ya Ardhi “Master Plan” ya eneo la Iwambi ikiwa ni sehemu ya mpango wa miaka 20 ya upanuzi wa Kampasi hiyo.

 “Nimefurahi sana kuona mpango wa matumizi ya ardhi Iwambi kwa ajili ya upanuzi wa Kampasi ya Mbeya. Natamani sana kuona mpango huu ukitekelezwa na nipo tayari wakati wowote kutoa mchango wangu wa mawazo ili mpango huu uweze kutekelezwa kwa manufaa mapana ya wananchi wa Nyanda za Juu Kusini na Nchi jirani zinazotuzunguka” Alisisitiza

 Ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya kuagana na wafanyakazi baada ya kutumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 11 tangu alipoteuliwa, amewapongeza Wafanyakazi na Wanafunzi kwa ushirikiano, na kwa kufanya kazi kwa bidii, kiasi cha kupelekea mafanikio makubwa katika kipindi kifupi, ikiwemo kuongeza idadi ya wanafunzi na programu zinazofundishwa chuoni hapo, pamoja na upanuzi wa miundombinu ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa jengo la Taaluma na  Utawala na jengo la  Maktaba.

 Wakimwelezea kwa nyakati tofauti Wanafunzi na Wafanyakazi wa Kampasi ya Mbeya wamesifu na kupongeza umahiri wa Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta katika kusimamia maendeleo ya chuo hicho, na kwamba amekuwa chachu ya maendeleo ya haraka na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kifupi cha uongozi wake.  

 Mhe. Barnabas Samatta, yuko kwenye ziara ya kutembelea chuo hicho, kukagua maendeleo ya kitaaluma na ujenzi wa miuondombinu, ziara aliyoianza 23 Julai 2020, Kampasi Kuu Morogoro na atahitimisha Kampasi ya Dar-es-salaam kwa kukagua upanuzi wa miundombinu, shughuli za kitaaluma pamoja na kuzungumza na Wanafunzi na Wafanyakazi.

                               *************************************************************************

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Barnabas Samatta akisalimiana kwa staili yake na mmoja wa viongozi wa Serikali ya wanafunzi (MUSO -Mbeya ) mara alipowasili chuoni hapo kwa ziara ya kikazi.

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe akiwa ameambatana na Mkuu wa Kampasi ya Mbeya Prof. George Shumbusho na Menejimenti ya Chuo hicho wakati wa kukagua jengo jipya la Taaluma na Utawala lililokamilika hivi karibuni.

Mkuu wa Chuo akiwa amekalia moja ya viti yanavyotumiwa na wanafunzi katika jengo jipya la Taaluma na Utawala, lililokamilika na kuanza kutumika. Wakishuhudia tukio hilo ni Makamu Mkuu wa Chuo hicho na Mkuu wa Kampasi ya Mbeya Prof. George Shumbusho.

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Barnabas Samatta akizungumza na wanafunzi (hawapo pichani) wakati alipofanya ziara kukagua shughuli za maendeleo Kampasi ya Mbeya.

Wakiwa kwenye picha ya pamoja nje ya jengo jipya ni Menejimenti, Wafanyakazi wa Kampasi ya Mbeya na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta, baada ya kukamikisha ziara yake chuoni hapo.

Address

MBEYA CAMPUS COLLEGE
Forest Area - Mbeya City
Mzumbe University
P.O.Box  6559, Mbeya, Tanzania
Tel: +255 (0) 252502863 /57/58
Fax: +255 (0) 252502862
email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.