WANACHUO NDAKI YA MBEYA WATAKIWA KUZIISHI TUNU ZA CHUO KIKUU MZUMBE

 
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha akiambatana na sehemu ya Menejimenti ya Chuo hicho kutoka Kampasi Kuu, wamefanya ziara ya kikazi Ndaki ya Mbeya leo tarehe 22 Aprili, 2024 na kuongea na Menejimenti na wanafunzi kwa lengo la kujadiliana masuala ya kimkakati pamoja na maendeleo ya chuo hicho.
Pamoja na mambo mengine kupitia ziara hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo pia amepata fursa ya kusikiliza changamoto zinazoikabili Ndaki ya Mbeya na jinsi ya kuzitatua.
 
Akizungumza na Wakuu wa Idara wa Ndaki ya Mbeya, Prof. Mwegoha amesisitiza kuhusu uwajibikaji na kuziishi tunu za Chuo Kikuu Mzumbe ikiwa ni pamoja na uwajibikaji, weledi, uwazi na kusimamia misingi ya haki katika utoaji wa elimu.
“Wakuu wa Idara mna kazi kubwa sana katika Chuo chetu, mnabeba dira na dhima ya chuo; hivyo, mna kila sababu ya kuhakikisha malengo yaliyopo katika mpango mkakati wa Chuo yanatekelezeka” Amesisitiza Prof. Mwegoha.
 
Prof. Mwegoha ametoa rai kwa wakuu wa Idara kusimamia misingi ya kazi kwa kuzingatia viwango vya ubora katika maeneo yote hasa kwa watu wanao wanaowaongoza.
Vilevile, amesisitiza kuandaa na kuchapisha maandiko mengi ya kitaaluma na kuwahamasisha kujisajili katika kurasa na majarida ya kimataifa ili kazi zao ziweze kuonekana duniani kote.
Katika ziara hiyo, Prof. Mwegoha amezungumza pia na wanachuo wa Ndaki ya Mbeya na kuwataka wanachuo hao kuzitumia vizuri tunu za Chuo hicho zinazojikita kwenye uwazi,Uwajibikaji, Ubunifu, Uadilifu na Heshima kwa kutoa ushirikiano na mrejesho kuhusu huduma zitolewazo na Chuo kukuu Mzumbe.
 
Akifafanua kuhusu tunu ya ubunifu, Prof. Mwegoha amesema Chuo Kikuu Mzumbe kitaendelea kubuni kozi zinazoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa na kuleta mawazo mengi ya kibunifu na kutumia vipaji walivyonavyo kuwekeza katika ubunifu ili kuleta manufaa ya Chuo na Taifa kwa ujumla.
Katika kikao hicho, Makamu Mkuu wa chuo alifafanua utekelezaji wa mpango mkakati wa Chuo hususani kipengele cha uendelezaji wa miundombinu na uboreshaji wa mazingira ya kujifunza na kufundishia pamoja na kutoa fursa kwa wanachuo kuwasilisha changamoto zao mbalimbali ambazo zilijibiwa na wajumbe wa timu ya Menejimenti.

 

Address

MBEYA CAMPUS COLLEGE
Forest Area - Mbeya City
Mzumbe University
P.O.Box  6559, Mbeya, Tanzania
Tel: +255 (0) 252502863 /57/58
Fax: +255 (0) 252502862
email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.